Mtanzania anaecheza soka la kulipwa nchini Hispania Farid Musa, ameendelea kufanya vizuri kwenye klabu yake ya Tenerife B inayocheza ligi ya vijana.
Farid amefunga magoli matano (5) katika mechi 12 alizoichezea timu hiyo huku akiwa amepiga pasi za mwisho ‘assists’ sita (6).
Nyota huyu ambaye anaichezea pia Taifa Stars alisajiliwa na Tenerife akitokea Azam FC lakini alipelekwa kwenye kikosi cha vijana ili kujifunza aina ya soka pamoja na mifumo mbalimbali inayotumiwa na klabu hiyo kabla ya kuanza kucheza kwenye kikosi cha wakubwa.
“Nimeanza kupata nafasi kwenye kikosi B lengo likiwa ni kufundishwa aina ya soka lao na mifumo wanayoitumia ili nikianza kucheza kwenye timu ya wakubwa kusiwe na kazi kubwa ya kuelekezwa nini natakiwa kufanya,” alisema Farid alipoitwa kwenye kikosi cha Stars kilichocheza mechi mbili za kirafiki za kimataifa dhidi ya Botswana na Burundi.
Shaffihdauda.co.tz inaungana na wadau wengine wa soka kumtakia kila la heri kijana Farid Musa katika kuipeperusha bendera ya Tanzania nchini Hispania.
0 comments