Open top menu
Alhamisi, 11 Mei 2017



SeeBait
Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kusini Mhe. Jacob Gedleyihlekisa Zuma amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali yake ya Awamu ya Tano kwa kuanza ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) na ameahidi kuunga mkono ujenzi huo.

Mhe. Rais Zuma ametoa kauli hiyo wakati wa mazungumzo rasmi na alipokuwa akizungumza na wananchi wa Tanzania na Afrika Kusini kupitia vyombo vya habari Ikulu Jijini Dar es Salaam, ikiwa ni katika ziara yake rasmi ya kiserikali ya siku mbili hapa nchini kwa mwaliko wa Mhe. Rais Magufuli.

Mhe. Rais Zuma amesema anatambua kuwa ujenzi wa reli ya kati utaleta manufaa makubwa kwa Tanzania na nchi za maziwa makuu na hivyo amekubali ombi la Mhe. Rais Magufuli la kuwahamasisha wafanyabiashara na wawekezaji wa Afrika ya Kusini kushirikiana na Tanzania kufanikisha mradi huo mkubwa.

Wakiwa katika Mazungumzo rasmi viongozi hao wamezindua rasmi Tume ya Pamoja ya Marais (Bi-National Commission-BNC) kwa kufanya kikao cha kwanza cha tume hiyo tangu ianzishwe mwaka 2011 ambapo wamepokea makubaliano yaliyofikiwa katika kikao cha tume ngazi ya mawaziri.

Kabla ya kuzungumza na wananchi kupitia vyombo vya habari Mhe. Rais Magufuli na Mhe. Rais Zuma wameshuhudia utiaji saini wa hati tatu za ushirikiano kati ya Tanzania na Afrika Kusini ambazo ni Muhtasari wa makubaliano ya mkutano wa tume ya pamoja ya Marais, Makubaliano ya ushirikiano katika masuala ya bioanuwai na uhifadhi na makubaliano ya ushirikiano katika sekta ya uchukuzi.

Akizungumzia makubaliano na mazungumzo yao Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mhe. Rais Zuma kwa kuitikia mwaliko wake na kukubali kuendeleza na kuongeza zaidi ushirikiano na uhusiano kati ya nchi yake na Tanzania hususani kuwahimiza wawekezaji na wafanyabiashara kuja kuwekeza nchini Tanzania katika sekta mbalimbali zikiwemo Kilimo, ujenzi wa miundombinu, utalii, madini na afya kwa kutumia uwezo mkubwa uliopo Afrika Kusini.

Mhe. Rais Magufuli amesema hivi sasa biashara kati ya Tanzania na Afrika Kusini kwa mwaka ni Shilingi Trilioni 2.4, uwekezaji wa Afrika Kusini hapa nchini ni Dola za Marekani Milioni 803.15 uliozalisha ajira 20,916 na kwamba kiwango hicho kinaweza kuongezeka zaidi endapo ushirikiano utaimarishwa zaidi.

“Na ili tufanikiwe kukuza biashara tumekubaliana kuondoa vikwazo na kuwahamasisha wafanyabiashara na wawekezaji wa nchi zetu mbili kutumia fursa ya uhusiano na ushirikiano mzuri wa kirafiki na kidugu uliopo kati ya nchi zetu kufanya kazi pamoja” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.

Mhe. Dkt. Magufuli ameongeza kuwa Tanzania itapeleka walimu wa lugha ya Kiswahili ambayo inazungumzwa na watu takribani milioni 120 ili wakafundishe lugha hiyo katika vyuo vya Afrika ya Kusini na hivyo kuimarisha zaidi ushirikiano.

Kwa upande wake Mhe. Rais Zuma amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kumualika kufanya ziara rasmi ya kiserikali hapa nchini na amesema nchi yake itahakikisha makubaliano yote ya Tume ya Pamoja ya Marais yanatiliwa mkazo na kutekelezwa kwa kuzingatia muda uliopangwa.

Mhe. Rais Zuma amesema Afrika Kusini inatambua na kuheshimu mchango wa mkubwa wa Tanzania kwa ukombozi wa nchi mbalimbali za Afrika ikiwemo Afrika Kusini ambayo Hayati Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere alishirikiana na Waasisi wa Taifa hilo walioongozwa na Hayati Mzee Nelson Mandela kupigania ukombozi na uhuru na kwamba anafurahi kuona Tanzania bado inatoa mchango mkubwa kupigania amani katika bara la Afrika.

“Mhe. Rais Magufuli naomba nikuhakikishie kuwa Afrika Kusini itaendeleza na kuimarisha zaidi uhusiano wake na ndugu na marafiki zake Tanzania katika kujenga uchumi kwa manufaa ya wananchi na pia kupigania amani kwa kuwa bila amani na usalama hakuna maendeleo” amesema Mhe. Rais Zuma.

Pamoja na kufanya mazungumzo rasmi, viongozi hawa watashiriki mkutano wa wafanyabiashara wa Tanzania na Afrika Kusini (Business Forum) unaofanyika katika ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere na jioni Mhe. Rais Zuma atahudhuria dhifa ya kitaifa iliyoandaliwa kwa heshima yake na mwenyeji wake Mhe. Rais Magufuli Ikulu Jijini Dar es Salaam kabla ya kurejea Afrika Kusini baadaye leo.
Tagged
Different Themes
Written by Lovely

Aenean quis feugiat elit. Quisque ultricies sollicitudin ante ut venenatis. Nulla dapibus placerat faucibus. Aenean quis leo non neque ultrices scelerisque. Nullam nec vulputate velit. Etiam fermentum turpis at magna tristique interdum.

0 comments